Na. John B. R. Chua (Wakili)
Simu: +255 692 880 644
Pengine umeona tangazo mtandaoni au hata kwenye mnada wowote kuwa kuna gari au piki piki inauzwa, gari au piki piki ambayo tayari imekwisha kuingizwa nchini Tanzania na kutumika kwa miaka kadhaa.
Mara nyingi watu wengi hupendelea kuuza magari au piki piki zao kupitia madalali ambao huweka matangazo kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii kama vile facebook au Instagram.
Je, umewahi kujiuliza ni mambo gani unapaswa kuyazingatia kabla haujanunua gari au piki piki ambayo tayari ina usajili wa Tanzania?
Kama umewahi kujiuliza swali hili na hukupata majibu bado unahita kufahamu zaidi basi leo nitakueleza mambo 5 muhimu kisheria ambayo unapaswa wewe kama mnunuzi mtarajiwa kuyafahamu kabla haujafanya maamuzi ya kununua gari au piki piki ambayo tayari ina usajili wa Tanzania.
Kabla ya kuanza kuyaangalia mambo hayo ni muhimu kufahamu kuwa biashara ya ununuzi wa gari au piki piki kama ilivyo kwa biashara nyingine nyingi huzalisha mahusiano ya kimkataba kati ya muuzaji au mmiliki na mnunuzi.
Sasa basi baada ya kufahamu kuwa biashara hii hujenga mahusiano ya kimkataba basi tuangalie mambo 5 muhimu yakuzingatia pindi unaponunua gari au piki piki iliyokwisha kusajiliwa Tanzania.
1. Hakiki umiliki wa muuzaji.
Hili ni jambo la kwanza kabisa la kuzingatia kabla haujafikia uamuzi wa kununua gari au piki piki ambayo tayari imekwisha sajiliwa nchini Tanzania. Namna gani utaweza kufahamu mmiliki halali wa gari au piki piki hiyo ni kwa kupitia kadi halisi ya gari au piki piki husika.
Hapa utamuomba muuzaji akupatie au akuoneshe kadi halisi ya gari au piki piki inayouzwa na wewe utaangalia mmiliki wa gari au piki piki hiyo ni nani kwa kusoma jina la mtu au taasisi litakalokuwa limeandikwa upande wa kulia wa kadi ya gari au piki piki.
Baada ya kufahamu majina ya mmiliki utamuomba muuzaji akupatie kitambulisho chake cha taifa au leseni ya udereva ili uweze kuhakiki majina yake kama ndio majina yaliyopo kwenye kadi halisi ya gari au piki piki inayouzwa. Kama ni gari au piki piki inayomilikiwa na taasisi au kampuni basi itakupasa uweze kuonana na wamiliki wa kampuni au viongozi wa taasisi hiyo ili kuhakiki kwanza taarifa za kuuzwa kwa gari au piki piki husika pamoja na azimio lililopitishwa na kikao cha wamiliki au viongozi wa taasisi husika kuridhia kuuzwa kwa gari au piki piki inayouzwa.
Baada ya kuhakiki majina yaliyopo kwenye kadi halisi ya gari au piki piki inayouzwa na kuona kuwa yanafanana au ndio haliyopo kwenye kitambulisha cha taifa au leseni ya udereva ya muuzaji basi hapo unaweza kuendelea na hatua nyingine za ununuzi wa gari au piki piki hiyo kwa kuzingatia mambo yanayofuata hapo chini. Ikiwa majina hayafanani na yaliyopo kwenye kadi ya gari au piki piki inayouzwa basi unatakiwa kufahamu kuwa huyo anayeuza gari au piki piki hiyo sio mmiliki wa chombo hicho hivyo hana uwezo wa kuuza au kukuuzia gari au piki piki hiyo.
Ikiwa gari au piki piki unayotaka kununua imetangazwa na dalali au mfanyabiashara anayeuza magari basi unapaswa kufahamu kuwa dalali au mfanyabiashara wa magari anajukumu la kukukutanisha na mmiliki halali wa gari au piki piki inayouzwa na wewe una wajibu wa kuhakiki umiliki wake kabla ya kununua gari au piki piki inayouzwa. Mauziano yatakayofanyika yatakuwa ni kati yako wewe mnunuzi na mmiliki halali wa gari au piki piki inayouzwa.
Endapo utanunua gari au piki piki kutoka kwa mtu ambaye sio mmiliki halali wa gari au piki piki hiyo tambua kuwa unaweza ukahusishwa na uhalifu mfano biashara haramu ya kuiba na kuuza magari yaliyoibiwa hivyo haishauriwi kabisa kununua gari au piki piki kutoka kwa mtu ambaye sio mmiliki wa gari au piki piki hiyo.
2. Ifahamu historia ya gari au piki piki husika.
Kabla ya kununua gari au piki piki ambayo tayari imeshasajiliwa Tanzania ni muhimu sana kuifahamu historia ya gari au piki piki hiyo. Hapa tunaposema ifahamu historia tunamaanisha historia ya umiliki pmoja na mwenendo wa gari au piki piki inayouzwa.
Inakupasa kufahamu gari au piki piki inayouzwa kwanza ni kwanini inauzwa pili inakupasa kufahamu kama gari au piki piki inayouzwa haijawahi kuhusishwa na matukio ya kiuhalifu, hapa utafahamu kwa kupitia uhakiki utakaofanywa na jeshi la polisi.
Watu wengi huwa hawafanyi uhakiki huu au hawaulizi juu ya historia ya gari au piki piki inayouzwa, pengine ni kwakutokufahamu madhara ya kununua gari au piki piki iliyohusishwa na matukio ya kiuhalifu mfano kusafirisha madawa ya kulevya, nyara za serikali au matukio ya uporaji na ujambazi.
Ikiwa utanunua gari au piki piki inayohusishwa na matukio ya uhalifu athari ambazo zinaweza kukupata ni pamoja na wewe binafsi kuhusishwa na magenge ya uhalifu jambo ambalo linaweza kusababisha ukahukumiwa kifungo jela pia kutaifishwa kwa gari au piki piki uliyoinunua bila kufahamu historia yake.
Hapa tunaona madhara ni makubwa sana na kwa bahati mbaya watu wengi huishia kwenye kukagua injini na vifaa vingine vya gari au piki piki na sio kukagua historia ya gari au piki piki inayouzwa.
3. Uwezo wa kufanyika uhamisho wa umiliki.
Ni muhimu kuweza kufahamu kama gari au piki piki inayouzwa inaweza kufanyiwa uhamisho wa umiliki bila kukupa usumbufu usio wa lazima.
Yapo mambo mengi yanayoweza kusababisha kushindwa kufanyika kwa uhamisho wa umiliki wa gari au piki piki iliyouzwa. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kutokukamilika kwa nyaraka za mauzo pamoja na nyaraka zinazopaswa kuambatanishwa na maombi ya uhamisho wa umiliki.
Mfano gari linalouzwa na msimamizi wa mirathi ya marehemu ni sharti nyaraka za kuteuliwa msimamizi wa mirathi na taratibu zote za kimahakama ziwe zimekamilika na kusiwe na wasi wasi wa kuzuka migogoro itakayopelekea kusimamishwa kwa zoezi la uhamisho wa umiliki.
Ili uweze kufahamu kama gari au piki piki husika inaweza kufanyiwa uhamisho ni vizuri kumuuliza Wakili anayekusimamia kwenye zoezi la kununua gari au piki piki inayouzwa ili aweza kukupa ushauri wa kisheria juu ya namna uhamisho wa umiliki utakavyofanyika na utachukua wastani wa siku ngapi kukamilika.
Hapa unapaswa kufahamu kuwa mara baada ya kununua gari au piki piki ni sharti na takwa la kisheria kufanya uhamisho wa umiliki, na anayepaswa kufanya uhamisho wa umiliki wa gari au piki piki iliyouzwa ni mmiliki halali wa gari au piki piki iliyouzwa. Ikiwa utaona uwezekano wa kufanyika kwa uhamisho wa umiliki wa gari au piki piki inayouzwa haupo basi ni vyema usinunue gari au piki piki hiyo hadi pale uwezekano wa uhamisho wa umiliki utakapokuwepo.
4. Historia ya kikodi pamoja na aina ya usajili wa gari au piki piki inayouzwa.
Ni muhimu sana kufahamu historia ya kikodi ya gari au piki piki unayotaka kununua. Taarifa za kikodi za gari au piki piki inayouzwa unaweza kuzipata kutoka kwa mmiliki au mamlaka ya kodi kwa kufanya uhakiki wa kikodi wa gari au piki piki inayouzwa.
Hapa tutaongelea zaidi historia ya kikodi inayoambatana na aina ya usajili wa gari au piki piki inayouzwa kwani yapo magari au piki piki ambazo ziliingia nchini kwa misamaha ya kodi hasa magari au piki piki zinazotumiwa na mashirika ya kimataifa, mashirika ya kidini au magari na piki piki zinazotumika kwenye miradi mbali mbali ya kijamii.
Ni muhimu kufahamu historia hii ya kikodi na usajili wa gari au piki piki inayouzwa. Ikiwa utaweza kufahamu historia ya kikodi na aina ya usajili wa gari au piki piki inayouzwa itakusaidia kuweza kupanga bei ya mauziano na mmiliki au muuzaji wa gari au piki piki inayouzwa, endapo gharama za uhamisho wa umiliki zitakuwa zinalipwa na wewe mnunuzi.
5. Shirikisha Wakili katika hatua zote za manunuzi hadi uhamisho wa umiliki.
Wakati unaponunua gari au piki piki inayouzwa ni muhimu sana kumhusisha Wakili tangu mwanzo wa ununuzi hadi hatua ya mwisho ya uhamisho wa umiliki. Hii itakusaidia kufahamu mambo mengi ambayo pengine usingeweza kuyafahamu au kuyazingatia wakati unanunua gari au piki piki ambayo tayari imeshasajiliwa Tanzania.
Watu wengi wamekuwa wakitafuta huduma au msaada wa Wakili pale ambapo tayari wameshapata tatizo hivyo kufanya gharama za kupata huduma ya Wakili kuwa kubwa zaidi na hata uwezekano wakufanikiwa kuzidi kupungua.
Mfano, pale ambapo utakuwa umenunua gari au piki piki ambayo imehusishwa na matukio ya uhalifu utajikuta unatafuta Wakili ili aweze kukutetea usikutwe na hatia ya kushiriki kwenye uhalifu na hata chombo chako kisitaifishwe au hata uweze kufidiwa endapo gari au piki piki uliyonunua itataifishwa.
Gharama za kuweza kufanikisha yote hayo ni kubwa na zinachukua muda mrefu, tofauti na kama ungemhusisha Wakili tangu mwanzo ulipohitaji kununua gari au piki piki iliyosajiliwa Tanzania.
Ni Imani yangu kuwa utakuwa umejifunza jambo jipya na pale utakapokuwa unataka kununua gari au piki piki ambayo tayari imesajiliwa Tanzania utayazingatia mambo haya 5 muhimu kisheria pamoja na mengine mengi yanayohusu ubora, thamani na uimara wa gari au piki piki unayotaka kununua ambayo sio sehemu ya taaluma yangu hivyo nakushauri pia kutafuta mtaalamu wa ufundi wa magari na piki piki ili aweze kukushauri juu ya masuala ya kiufundi yanayohusiana na gari au piki piki unayotaka kununua.